Wamevuna walichopanda Ligi Kuu

0
Spread the love

Baada ya ligi kumalizika, kila timu imevuna ilichopanda, kwani kila iliyofika kwenye nafasi iliyopo, ndiyo mavuno ya msimu mzima kwa jinsi ilivyojiandaa.

Spread the love

Safari ndefu ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2022/23 ilitamatika mwezi huu, wakati timu zote 16 zilipomalizia raundi ya 30 na kukaa pale zilipostahili.


Ligi hiyo iliyoanza Agosti 15 mwaka jana, ithitimishwa kwa bingwa Yanga kukabidhiwa mwali wao mpya aliyetambulishwa na wadhamini wa Ligi Kuu hivi karibuni.
Baada ya ligi kumalizika, kila timu imevuna ilichopanda, kwani kila iliyofika kwenye nafasi iliyopo, ndiyo mavuno ya msimu mzima kwa jinsi ilivyojiandaa.


Ukiacha ubingwa, kuna timu zilizopata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho, zilizosalia, zitakazokwenda kucheza mchujo ‘play off’ na ambazo zimeipa mkono wa kwaheri ligi hiyo, hivyo kutoonekana tena msimu ujao.
Mwandishi wa makala haya amechambua ushiriki wa timu zote kwenye ligi hii msimu mzima.


1. Yanga

Yanga wakisherehekea kubeba taji la Ligi Kuu (Hisani/Yanga)


Haikushangaza sana kutwaa tena ubingwa kwa mara ya pili kutokana na viwango vya wachezaji wao, upambanaji, kujituma, mbinu za kocha wao Mtunisia Nasreddine Nabi, pamoja na kuwa na kikosi kipana.
Yanga ni moja kati ya timu chache kwenye Ligi Kuu iliyokuwa na wachezaji wanaocheza na waliokaa benchi wenye viwango vinavyofanana, au kukaribiana.
Hata hivyo kuna sehemu ambayo wengi wanairuka na kutoipa pongezi, nayo ni eneo la kocha wa viungo wa timu hiyo. Yanga imetwaa ubingwa na kufika hata kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho kutokana na pia na ufiti, au utimamu wa mwili wa wachezaji wake, ambao karibia wote, wanaoanza na walio benchi walionekana wako timamu kimwili hata pumzi. Msimu huu imetwaa ubingwa ilimaliza na pointi 78, nne zaidi ya msimu uliopita ilipomaliza na pointi 74.

2. Simba

Kuna vitu vichache tu ambavyo vimeifelisha Simba msimu huu. Ukiangalia takwimu karibia zote zinawabeba. Imefunga mabao 75 ambayo ni mengi zaidi kuliko timu yoyote, ikiruhusu mabao 17, machache zaidi kuliko timu zote. Hata pointi ilizomaliza nazo ni 73,  ambazo ni 12 zaidi kuliko za msimu uliopita ilipomaliza na pointi 61 tu.
Ufinyu wa kikosi kwa kiasi kikubwa uliinyima ubingwa, kwa sababu ilikuwa na wachezaji wa kikosi cha kwanza tu, wachezaji wa benchi hawakuwa na viwango kinavyokaribiana baadhi ya hata nusu na wenzao.
Wachezaji Joash Onyango na Clatous Chama kwa nyakati tofauti, pia wazilitaja mechi dhidi ya Azam ya mzunguko wa kwanza waliopoteza kwa bao 1-0 na sare ya mabao 2-2 dhidi ya KMC ilizitoa timu hiyo kwenye reli. Faraja pekee ni kwamba imepata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao

3. Azam FC

Imekamata nafasi ya tatu kama kawaida yake, safari hii ikikusanya pointi 59, ambazo ni 10 zaidi ya zile za msimu uliopita ilipomaliza na pointi 49. Imefanikiwa kukata tiketi ya kucheza mechi za Shirikisho la Soka Afrika msimu ujao. Zaidi ya hapo haikuwa na cha ajabu sana zaidi ya ilivyokuwa kwenye ligi zilizopita.

4. Singida Big Stars

Ni timu iliyoanza kucheza Ligi Kuu msimu huu na moja kwa moja inakwenda kushiriki Kombe la Shirikisho barani Afrika. Pamoja na hayo, matokeo mazuri iliyokuwa inayapata hayakuwashangaza mashabiki wa soka kutokana na aina ya wachezaji iliyokuwa nayo, na wale ambao imewasajili. baadhi wameonyesha uwezo mkubwa na wengine ni wazoefu kutoka klabu kubwa, hususan Simba na Yanga.

5. Namungo FC

Imemaliza kwenye nafasi ya tano kama ilivyokuwa msimu uliopita. Hata hivyo msimu huu imepungua kasi, kwani imemaliza mechi 30 ilipata pointi 40, wakati msimu ulipota ilimaliza idadi ya mechi hizo ikiwa na pointi 41.
Baada ya kutofanya vema msimu uliopita, ilitegemewa msimu huu ingekuwa na nguvu mpya, lakini iliendelea kuwa ni ile ile ya msimu iliopita na si ya kutisha ya misimu miwili nyuma.

6. Ihefu SC

Hii ni moja kati ya timu iliyowashangaza mashabiki wengi wa soka. Imepanda daraja msimu huu, baada ya kuteremka msimu wa 2020/21.
Hadi mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu unamalizika, ilikuwa inahesabika kuwa itakuwa moja ya timu zitakazoshuka daraja. Ilibadilika na kuwa tishio mzunguko wa pili hasa baada ya kupata wachezaji wa mkopo kutoka klabu za Simba na Yanga, hadi kumaliza ikiwa ya sita. Kwa maana hiyo msimu huu hakuna timu iliyopanda na kushuka moja kwa moja.

7. Geita Gold

Haikuwa kama ile ya msimu uliopita, iliyomaliza wa nne na kucheza Kombe la Shirikisho barani Afrika. Haikuwa na msimu mzuri sana, hivyo imemaliza ikiwa ya saba, ingawa haikuwa na tishio lolote la kutaka kushuka daraja. Ilichanga karata zake vizuri na ikawa kwenye nafasi ya katikati ya msimamo kwa muda wote wa ligi.

8. Prisons

Msimu uliopita ilinusurika kwenye mechi za mchujo ‘play off’, ikizuia kupata JKT Tanzania na kubakia Ligi Kuu. Inaonekana kuwa somo liliwaingia. Hata hivyo, mpaka mzunguko wa kwanza unamalizika ilikuwa hoi bin taaban. Ilibadilisha nafasi ya Ihefu kule mkiani. wakati Ihefu ikishtuka mapema mwanzoni tu mwa mzunguko wa pili, Prisons ilianza kugangamala katikati ya mzunguko huo, hasa baada ya ujio wa kocha Mohamed Abdallah ‘Bares’ na kuifanya kumaliza nafasi ya nane kwa pointi 37, badala ya nafasi ya 14 msimu uliopita ikimaliza na pointi 29.

9. Dodoma Jiji

Ni moja kati ya timu iliyojifunza kutokana na makosa ya msimu uliopita. Japo haikuwa kwenye nafasi nzuri sana, lakini imemaliza ikiwa na tisa, ikikusanya pointi 37 na kuwa na uhakika wa kubaki Ligi Kuu. Msimu uliopita ilimaliza ya 11, na pointi 35.

10. Mtibwa Sugar

Inaonekana kama ni timu iliyozoea kuzicheza karata zake vema kwenye mechi za mwisho. Msimu uliopita iliponyeka kwenye ‘play off’ dhidi ya Transit Camp, ikifungwa bao 1-0 ugenini, na kushinda 4-1 nyumbani. Ilimaliza nafasi ya 13 ikiwa na pointi 31. Msimu huu, pamoja na kwamba ilikuwa kwenye hali mbaya, lakini ilimaliza nafasi ya 10, pointi 35.

11. Kagera Sugar

Haikufanya vema msimu huu. Imemaliza nafasi ya 11 na pointi zake 35, wakati msimu uliopita ilimaliza ya sita, ikiwa na pointi 39.

12. Coastal Union

Imeponea chupuchupu kucheza ‘play off’ kama ilivyokuwa msimu uliopita iliponusurika dhidi ya Pamba FC. Safari hii imemaliza nafasi ya 12 na pointi 33.

13. KMC


Inawezekana tukawa nayo msimu ujao au la. Imeshika nafasi ya 13 kwenye msimamo na itakwenda kucheza ‘play off’ dhidi ya Mbeya City. Msimu iliopita ilimaliza kwenye nafasi ya 10.

14. Mbeya City

Kwa miaka ya karibuni imekuwa ni timu ya kusuasua kutoka timu tishio. Nayo itajaribu bahati yake dhidi ya KMC mechi ya ‘play off’.
Angalau msimu uliopita ilimaliza nafasi ya tisa na pointi 37.

15. Polisi Tanzania

Wala haikushangaza yoyote ilivyoshuka daraja. Ilionekana tangu mwanzo kuwa safari ingewakumba. Imemaliza ligi ikiwa na pointi 25 tu, wakati msimu uliopita ilimaliza kwenye nafasi ya nane ikiwa na pointi 37.

16. Ruvu Shooting

Ndiyo timu ya kwanza kushuka msimu huu. Kama alivyosema kocha wake mkuu Mbwana Makata aliyejiunga baadaye sana kwenye kikosi hicho kuwa tatizo lilianza kwenye usajili. Haikuwa na wachezaji wenye viwango na hata wakati wa dirisha dogo hakukuwa na fungu la usajili kiasi cha kuongeza mchezaji mmoja tu. Msimu uliopita ilishika nafasi ya 12.

About Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

P