Penati ya kizembe yamchefua Gamondi, amcharukia Zawadi Mauya

0

Kocha Miguel Gamondi

Spread the love

Bao la Tito Mayor wa AS Ali Sabieh (ASAS) ya Djibouti kwa mkwaju wa penalti dakika ya 85 limetibua rekodi ya Yanga kutoruhusu nyavu zake kutikiswa katika mechi rasmi msimu huu na kumsikitisha kocha Miguel Gamondi

Mabingwa hao wa Tanzania wamefanikiwa kufuzu Raundi ya mwisho ya mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya AS Ali Sabieh (ASAS) ya Djibouti katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.


Mabao ya Yanga leo yaliwekwa kimiani na winga Mkongo, Max Nzengeli dakika ya 7 na muda wa nyongeza kipindi cha pili, mshambuliaji Mghana Hafiz Konkoni dakika ya 45, kiungo Muivory Coast Pacome Zouazoua na mshambuliaji chipukizi wa Kimataifa wa Tanzania, Clement Mzize dakika ya 69, wakati bao pekee la ASAS limefungwa na Tito Mayor kwa penalti dakika ya 85.


Yanga imefuzu kwa ushindi wa jumla wa 7-1 na sasa itakutana na Al-Merreikh ya Sudan mechi ya kwanza wakianzia ugenini Septemba 15 na marudiano na Dar es Salaam Septemba 29.

Licha ya kufurahia kiwango kizuri kilichooneshwa na kikosi chake, kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amemlaumu kiungo wake, Zawadi Mauya kwa kufanya kosa la kizembe lililopelekea ASAS kupata penati iliyotibua rekodi ya kutimiza mechi tano za msimu huu bila kuruhusu bao.

“Sijafurahishwa kufungwa kwa penalti rahisi. Sio tu ishu ya mchezo wa leo, ikiwa unafanya makosa kama hayo unaweza pia kuyafanya katika mechi mgumu. Ni kosa kubwa, faulo isiyo ya lazima. Hata katika mechi moja ya mazoezi huko nyuma alifanya kitendo kama hicho. Tunahitaji kujifunza kutokana na makosa kwa sababu tumecheza mechi tano rasmi na tungeweza kuwa na clean sheet tano.”

Kiungo Zawadi Mauya aliyeingia kipindi cha pili alimkwatua mshambuliaji wa ASAS ndani ya eneo la hatari na kupelekea mwamuzi kuamuru mkwaju wa penati uliokwamishwa nyavuni na Mayor.

Kabla ya kuruhusu bao dhidi ya ASAS, Yanga ilikuwa imecheza mechi mbili katika Ngao ya Jamii na kushinda 2-0 dhidi ya Azam na kisha kupata sare ya 0-0 dhidi ya Simba licha ya mechi kuamuriwa kwa sheria ya matuta baada ya dakika 90.

Katika Ligi Kuu, Yanga imecheza mechi moja na kuvuna ushindi mkubwa wa mabao 5-0 dhidi ya KMC. Kabla ya kuivaa KMC, Yanga iliichapa ASAS mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

About Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

P