Mataji tu ndani ya Yanga hayatoshi kumpa Nabii maua

0
Spread the love
Nabi katika majukumu yake dimbani (Picha/Yanga SC)

Nasreddine Nabi ameifikisha Yanga kileleni, ni ngumu kusalia hapa, ni ngumu zaidi kwenda mbele zaidi ya hapa. Angeweza kusalia na kufanya vizuri lakini kihesabu ni rahisi kushusha heshima kuliko kuilinda. Yaliwahi kumtokea Claudio Ranieri aliyetimuliwa msimu mmoja baada ya kufanya moja ya miujiza mikubwa kuwahi kushuduhiwa katika ulimwengu wa soka alipoiongoza Leicester City kutwaa taji la Ligi Kuu Uingereza msimu wa 2015/16.

Turudi nyuma kidogo, Nabi alikaribishwa kwa salamu za kupokea kipigo kutoka kwa Azam. Baada ya kupoteza mchezo huo ni kama alishtuka, kukuna kichwa na kusaka suluhisho lililopeleka kucheza mechi 49 za Ligi Kuu Tanzania Bara bila kupoteza. Rekodi tamu na ya kukumbukwa hadi itakapovunjwa.

Kipi kilichomtofautisha kocha Nabi au tutamkumbuka kwa kitu gani akiwa Yanga?

Kwanza, Nabi alijipambanua  namna alivyoweza kuishi na kukiongoza kikosi chake. Wachezaji wa Yanga hawakumuita ‘Baba Nabi’ kwa amri bali muitikio wa pamoja uliotokana na kutambua jinsi alivyowachukulia kama watoto wake wanaohitaji muongozo, kusikilizwa changamoto zao za kibinadamu, kukosoloewa panapohitajika, kupongozewa wanapofanikiwa na kutiwa moyo wanapojikwaa katika maisha ya kila siku ndani na nje ya uwanja.

Kinywa cha Nabi kilikiri nguzo kuu ya mafanikio ni namna ya kuishi na wachezaji ili wote wajione wana mchango katika klabu na alilifanikisha kwa kupanga na kupangua kikosi chake mara kwa mara kuhakikisha kila mchezaji anapata dakika za kucheza kwa kadri inavyowezekana kulingana na matokeo, ratiba iliyopo na uwezo wake.

“Ili ufanikiwe kwenye soka siyo jambo la mbinu za uwanjani pekee, katika kusimamia na kufundisha wachezaji, jambo la kwanza ni kutengeneza mahusiano nao kama binadamu. Ni muhimu. Ubinadamu na mahusiano yana uzito zaidi ya mbinu za soka.”

Nabi pamoja na Fiston Mayele na Stephane Azizi Ki (Picha: Yanga SC)

Alitamka Nabi katika moja ya mazungumzo yake baada ya mechi ya Ligi Kuu baada ya kumshuhudia Stephane Azizi Ki aliyekuwa akipitia kipindi kigumu ndani ya uwanja akifunga mabao matatu.

Aliongezea, Siku zote ni usimamizi wa wachezaji, kuweka usawa katika kikosi kwa wachezaji kucheza kwa kupokezana kuhakikisha wachezaji wanabaki na kiu ya kutosha ya kujitoa kuipambania timu.”

Toleo bora la Feitoto

Jambo la  pili tunaloweza kulitafakari na kuchukua kutoka kwa Nabi ni namna alivyofanikiwa kuwapanga wachezaji katika maeneo sahihi kulingana na aina ya uchezaji wao na mahitaji ya mechi husika. Na hapa lazima tuchimbe ndani zaidi.

Feisal Salum maarufu kama “Fei Toto” licha ya huu ustaa wote, ila kabla ya Nabi alikuwa haeleweki anacheza nafasi gani na ubora wake ni upi na ndio maana aliwagawa mashabiki kutokana kuwepo na kundi kubwa lilioamini jina lake liliimbiwa zaidi kuliko kiwango na mchango wake uwanjani.

Nieleweke vizuri, sio kuwa Feitoto alikuwa anacheza vibaya kabla ya Nabi, La hasha bali alionekana kama mchezaji mzuri mwenye nyota ya kupendwa tu. Wenyewe wanasema kismati mjini.

Kuna waliokwenda mbali zaidi na kumuona ni mpaka rangi,  “backwards pass merchant ” yaani mtaalamu wa kurudisha mipira nyuma. Haishangazi Kocha wa Taifa Stars wakati huo, Emmanuel Amunike aliibuwa mjadala mzito aliposema Feitoto ni wa kiwango cha kucheza Barcelona.

“Feisal anapambana sana ni mchezaji anayejituma na anajua nini anapaswa kufanya akiwa uwanjani, kama ingekuwa Ulaya basi angecheza Barcelona,” alisema Amunike

Maji yalipozidi unga na kocha Amunike kulazimika kumpumzisha Feitoto kabla ya mwamuzi kupuliza kipenga cha kumaliza kipindi cha kwanza katika pambano dhidi ya Senegal kwenye Fainali za Kombe la Mataifa Afrika nchini Misri mwaka 2019, upele ulipata mkunaji kwa wale walioamini kijana kutoka Visiwa vya Marashi ya Karafuu anaimbwa kuliko uwezo wake na kusahau kama alicheza mechi ya AFCON akiwa na umri mdogo na pengine katika nafasi ambayo haikupi ubora wake halisi..

Hata hivyo Nabi alifungua utaalamu wake mara moja, akatuonesha toleo bora la Feitoto na kufunga mjadala wa ubora wa mchexaji huyo wa zamani wa JKU. Badala ya kumchezesha dimba la chini kama mmoja wapo wa viungo wa ulinzi, alimpandisha na kumcheza kama namba 10 nyuma ya mshambuliaji. Mambo yalibadilika, Feitoto aliyeimbwa kwa madoido akaanza kuonesha mchango usiopingika. Jina la Zanzibar Finest likaonekana kumfaa.

Kabla ya msimu kumalizika Feitoto alionesha kiwango bora sana na mechi aliyovuma ilikuwa dhidi ya Ihefu 2021 jijini Dar es Salaam alipofunga mabao mawili.

Msimu uliofuata 2021/22, Feitoto ndio alionekana kuimarika zadi katika nafasi hiyo ya namba 10, uongozi wa klabu hakuangaika kwenda kununua tena mchezaji katika nafasi waliyokuwa wanaumiza kichwa kusaka mtu atakayewafanya wajibu kelele za Simba waliokwa wanatamba na Clatous Chama, walifurahia uwepo wa mchezaji aliyegeuzwa na kupewa jukumu lililomfaa na matokeo yake kuongeza kicheko Jangwani. Ni Feitoto aliyewapa kiburi viongozi wa Yanga kumrushia virago Godfather wa Bujumbura bila mashabiki kuwapigia kelele.

Na sio tu Nabi alimboresha Feitoto kwa kugundua nafasi yake bora zaidi uwanjani bali kumuongezea ufanisi wa kujua kufanya mikimbio sahihi. Awali Feisal hakua mchezaji wa kuwa mbali na mpira lakini hasa msimu huu wa 2022 /23 hadi mgogoro wake na klabu ulipotokea na kumweka nje ya uwanja, alikuwa ameonesha mabadiliko makubwa kwa jinsi alivyokuwa hodari kukimbia na kufika kwenye eneo la mpinzani kwa muda sahihi na kuleta madhara makubwa yaliyofaidisha timu yake. 

Kama vile haitoshi, alimbadilisha tena na kuanza kumchezesha kama kiungo wa mbele anayeanza kama namba 8 na kumalizia kama namba 10 ndani ya kumi na nane siku akianza na  Stephane Aziz Ki, kitendo ambacho hakikumuondolea magoli miguuni wala kumunguzia pasi za mabao badala kikamuongezea zaidi ufanisi wake wa kunusa hatari.

Magoli yalifungwa na pasi za mabao zilizalishwa na Feitoto aliyevuma sana kwani ufanisi wake wa mashuti ulitokana na uwezo wa kufika katika eneo sahihi. Alihama kutoka mchezaji aliyependa kuwa eneo lenye mpira na kuwa mtu aliyejitenga na kuingia wa mwisho kwenye eneo la hatari, maarufu  kama ‘zone 14’ kitu kilichompa nafasi nzuri ya kuweza kuwa na ramani nzuri ya wapi aupeleke mpira na pia kuwahi pasi kutoka kwa wenzake au mpira inayoambaa.

Mayele vs Makambo

Mageuzi mengine ya Nabi yanaweza kuonekana katika washambuliaji wawili raia wa Kongo, Heritier Makambo na Fiston Mayele. Makambo alikuwa chaguo la kwanza la mashabiki kutokana na yale aliyoyafanya alipotua nchini kwa mara ya kwanza. Aliporudi alipokelewa kwa shangwe kubwa zaidi kuliko Mayele ambaye alikuwa ‘mtu asiyejulikana’ machoni mwa wengi.

Makambo alianza mechi tatu baada ya usajili wao ikiwemo mbili dhidi ya Rivers United ambazo Yanga walipoteza.

Mechi iliyofuata ilikuwa dhidi ya Simba kwenye Ngao ya Hisani, ufunguzi wa msimu wa 2021/22. Mayele alianza mbele ya Makambo, mashabiki walishtuka kumuona Mzee wa Kuwajaza akichoma mahindi mbele ya ‘mtu asiyejulikana’ tena katika mechi kubwa dhidi ya mtani.

Mayele analeta vitu tofauti sio magoli tu, namna ya kusukukumana na walinzi, kushikilia mipira, kuipa timu mtu wa kuwasaidia wakati wanajilinda hasa katika mipira ya juu. Mayele amekuwa na mafanikio makubwa, sio kwa kufunga mabao ndani na nje ya Tanzania ball kuwa mpaka mchezaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa 2022 na 23.

Kumpa uhai Kibwana

Kibwana Shomary ni mchezaji mwingine aliyepitia mageuzi makubwa kwenye mikono ya Nabi. Baada ya msimu wa kwanza ilionekana kama Kibwana licha ya juhudi zake bado sio mchezaji wa kiwango cha kuanza mechi katika kikosi cha kwanza. Kelele zilipigwa na viongozi waliitikia na kumleta Djuma Shaban kutoka AS Vita.

Ujio wa Djuma Shaban ulionekana kama mwanzo wa mwisho wa maisha ya Kibwana ndani ya Yanga. Hata hivyo Nabi alionesha utofauti na kumpa uhai mwingine Kibwana na kuendelea kuonekana lulu ndani ya kikosi cha Yanga.

Ni Nabi aliyeamua kumuamini kiasi cha kumchezesha nafasi ya beki wa kushoto licha ya  kuwa Kibwana ni mchezaji anayetumia mguu wa kulia. Aliweka pamba masikioni na kumchezesha katika mechi kubwa.

Kibwana hana kimo lakini uwezo wake mkubwa ni kwenye kujilinda, na anacheza nafasi ya beki wa kushoto kama kulia, ngumu kujua mguu anaotumia na kuonesha udhaifu kwa mshambuliaji na amekuwa na msimu mzuri sana ndani na nje ya Tanzania.  Pale Nabi anapotaka mechi kucheza kwa tahadhari, Kibwana alimuamini.

Somo jingine ni Ibrahim Bacca, alipotua kikosi hapo alisuburi kwa muda mrefu, lakini kama Nabi anavyotambulika kama “Profesa”  alitumia muda kumpika.

Ndani ya msimu huu dhidi ya US Monastir nyumbani Dar, Bacca ndiyo alianza mechi kubwa yake ya kwanza na sio maajabu ni kwamba lilikuwa pambano sahihi kwake na tangu hapo ameimarika na kuwa mzuri sana hasa katika kucheza upande mgumu wa eneo la beki wa kati wa kushoto licha ya kutumia mguu wa kulia.

Ameonesha uwezo mzuri hususani katika matumizi ya tackling, nguvu na uwezo mkubwa wa kuusoma mchezo na kufanya maamuzi sahihi kumkabili mpinzani.

Ubora wa mbinu na kubadili mipango

Mabadiliko yake ya wachezaji wakati wa mechi  yalikuwa ya mahesabu makali, sio kufanya mabdiliko kwa kuwa fulani ameonekana kupwaya basi abadilishwe. Aliangalia sababu, mwenendo wa mechi na muda sahihi, kila kitu kilikuwa kifanyike kwa usahihi na sio ilihali mabadiliko yamefanyika kisa matokeo si mazuri au tayari yamepatikana.

Nabi alitengeneza ukuta mzuri timu ikiwa haina mpira, tangu mchezo wake wa mwanzoni, timu ilicheza katika mfumo wa 4-4-2. Bila mpira, namba 10 na mshambuliaji mmoja walikuwa walinzi wake wa kwanza huku mawinga wakiungana na viungo wawili wa kati kupngeza kuimarisha usalama.

Nabi alikuwa hatabiriki, kuna baadhi ya mechi alishambulia kama kawaida kwa kutumia 4-2-3-1 na mechi nyingine 4-3 -3 hususani mwanzoni aliposajiliwa Salum Abubakar kutokea Azam.

Ilimaanisha Yannick Bangala alikuwa anacheza kiungo wa chini pekee, kisha Salum Abubukar pamoja na Feisal kama viungo wawili wa pembeni.

Msimu huu baada ya kupoteza dhidi ya US Monastir ugenini, mechi ya nyumbani dhidi ya Tp Mazembe aliachana na 4-2-3-1 na kwenda na 4-3 -3 akiwatumia Mudathir Yahya na Khalid Aucho kama namba 8 wawili na Bangala kama kiungo mkuu wa kati.

Mfumo huo ulimpa ulinzi tosha, huku akitaka namba nane wa karibu na mpira kuungana na Mayele kutia presha kwenye mpira.

Mbinu nyingine ni kucheza na walinzi watatu wakiwa na mpira na watano wakiwa hawana.

Hii mbinu aliitumia dhidi ya Simba katika nusu fainali ya kombe la shirikisho la Azam, fainali dhidi ya Coastal Union, dhidi ya USM Alger ugenini kwenye fainali ya kombe la shirikisho Afrika na dhidi ya Azam FC kwenye fainali ya kombe la shirikisho la Azam.

Na ulizaa matunda baadhi ya michezo na kuleta shida dhidi ya mpinzani kwani hawakutegemea Yanga kuingia kivile.

La mwisho, Nabi amekuwa akichukua muda kumuingiza mchezaji kikosini na hapendi kutiwa presha, namna alivyoweza kuonesha uongozi dhidi ya Stephane Aziz Ki ambaye amekuwa akionekana kutoendana na mipango ya timu mara kwa mara.

“Kwa mara nyingine niseme inabidi tumpe muda Azizi ili kuzoea timu. Inabidi tumvumilie. Ni mchezaji mzuri, anaweza kucheza nafasi yoyote mbele, ni suala la kutafuta njia sahihi ya kumpanga.”

Pale ambapo ameona hafai kuanza, amesisitizia hapo hapo kutoanza na pale anapoona anafaa amemuanzisha bila mtu yoyote kumuingilia. Joyce Lomalisa nae amechukua muda kwendana na kasi ya timu .

Kila mchezaji amekuwa akitumika katika mechi sahihi, timu imekuwa timu kweli na sio bila mchezaji  fulani timu haisogei. Nabi alitengeneza timu na sio bila mchezaji fulani kuwepo kwenye pambano la siku hio mashabiki wanaingia uwanjani na roho mkononi.

Mataji aliyobeba ni alama isiyofutika katika klabu Ya Yanga, lakini mageuzi yake ndani ya uwanjani na hasa namna alivyowabadili na kuwatumia wachezaji ndio vitu vya kumfanya tumkumbuke na kumuenzi zaidi daima. Mafanikio ya timu ikiwemo kubeba mataji mbalimbali ni juhudi za wadau mbalimbali  ikiwemo viongozi, mashabiki, wachezaji na benchi la ufundi lakini mbinu za uwanjani ni kitu binafsi cha kujivunia kutoka kwa kocha na hapa ndipo Nabi anastahili maua yake ya kipekee.

Kwa heri Nabi, asante kwa utumishi uliotuka ndani ya Yanga. Hakika soka la Tanzania limeongeza kitu kutoka kwako. 

About Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

P