February 25, 2024

Itakuwa fedheha kubwa Simba kushindwa kufuzu Makundi Ligi ya Mabingwa-Ahmed Ally

0
Spread the love

Afisa Habari wa Simba, Ahmed Ally amesema itakuwa ni fedheha kubwa kushindwa kufuzu hatua ya Ligi ya Mabingwa Afrika mbele ya Power Dynamos ya Zambia.

Ahmed amesema kwamba, Simba hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika sio malengo bali ni njia yao ya kusonga mbele zaidi kwenye mashindano hayo. Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuelezea mipango ya mechi yao hiyo dhidi ya Power Dynamos.

Fabrice Ngoma akiruka kupiga kichwa kuiandikia Simba bao la pili dhidi ya Power Dynamos timu hizo mbili zilipokutana kwenye mchezo wa kirafiki katika tamasha la Simba Day. (Picha: SimbaSC)

“Bahati nzuri au mbaya hawa Power Dynamos tumecheza nao hivi juzi tu hapa kwenye tamasha letu la Simba Day. Tukawafunga mabao 2-0 lakini lazima tuwe wakweli tusitegemee Power Dynamos tuliowaona kwenye tamasha ndio tutakaowaona wakiwa nyumbani kwao Levy Mwanawasa. Tusitegemee Power Dynamos waliocheza kwa kujiachia kwenye tamasha la Simba Day ndivyo watakavyocheza kwenye mechi ya kuwania kufuzu kuingia hatua ya Makundi ya Ligi ya Mbaingwa Barani Afrika.”

“Kwanza hawana historia nzuri na hatua nzuri ya hatua ya makundi. Wanataka kuandika historia yao, wanataka kutengeneza ufalme wao kwenye michuano ya kimataifa. Wanatuonea ndonge namna ambavyo tumekuwa na mafanikio kwenye michuano ya kimataifa.”

“Kwa hivyo watakuja kupambana kwa hali zote kuhakikisha wanafanya vizuri na kuingia kwenye historia ya kuingia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Lakini ni lazima wakumbuke sisi ni Simba Sports Club, hatua ya Makundi ni eneo letu la kujidai. Ni sehemu ambayo tukilalala, tukiamka tunaangukia Makundi. Itakuwa ni fedheha ya hali ya juu sana kwa Simba kushindwa kufuzu ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.”

“Lazima tuingie kwenye mchezo huu tukitambua kuwa tunayo dhima kubwa ya kutupeleka hatua ya Makundi. Sio kuwa tunataka kutimiza malengo ya kucheza hatua ya makundi. Hatua ya Makundi ni sehemu ya mapito yetu kuelekea kwenye malengo yetu. Wapo watu hayo ndio malengo yao. Yaani mtu ana miaka 80 malengo yake ni kucheza hatua ya Makundi. Sasa huyo sio Simba. Simba makundi tunapita, yaani ni njia ya kwenda tunakotaka kwenda.”

Simba itasafiri kwenda Zambia kuivaa Power Dynamos katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya raundi ya pili ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa Jumamosi ya tarehe 16 Septemba jijini Ndola katika uwanja wa Levy Mwanawasa.

About Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

P