February 25, 2024

Bakari Shime alia na uwanja kipigo dhidi ya Nigeria

0

Kikosi cha timu ya taifa ya wasichana chini ya umri wa miaka 20, Tanzanite Queens kilichoanza dhidi ya Nigeria.

Spread the love

Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya wasichana chini ya umri wa miaka 20, Bakari Shime, amesema uwanja wa Moshood Abiola jijini Abuja ulisababisha washindwe kucheza soka lao lililozoeleka na kusababisha kupokea kipigo dhidi ya Nigeria.

Tanzanite Queens imetupwa nje ya mbio za kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Colombia baada ya kufungwa mabao 2-1 na wenyeji, Nigeria katika mchezo wa marudiano Raundi ya Tatu kufuzu uliochezwa Uwanja wa Taifa wa Moshood Abiola Jijini Abuja siku ya Jumapili.

Kwa matokeo hayo, Tanzanite Queens imetupwa nje ya mashindano kwa kichapo cha jumla ya mabao 3-2 kufuatia sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyopita Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya mechi ya hio kutamatika, Shime alisema haikuwa rahisi kwao kucheza mpira wa pasi za chini kama kawaida yao na kulazimika kutumia pasi ndefu kwenye hali ile ya uwanja wa Abiola jinsi ilivyokuwa.

Hata hivyo, aliwasifu wachezaji wake kwa kuwa walicheza vizuri na kufuata maelezeko licha ya matokeo kutokuwa upande wao.

“ Kwanza kabisa niwapongeze wachezaji wetu kwa namna walivyocheza. Wamejitahidi kufuata maelekezo na wamecheza vizuri. Pia niwapongeze washindi kwa sababu kwa mipango yao wamepata matokeo mazuri ambayo yamewafanya wasonge mbele.”

“Yote kwa yote mechi ilikuwa na ushindani mkubwa. Mechi ilikuwa na upinzani katika muda wote wa mchezo. Tumecheza vizuri kwa maana ya kucheza kwa mipango yetu ingawa tulilazimika kubadili aina ya kucheza. Kiwanja hakikuwa rahisi sana, kilikuwa kinasumbua kuruhusu mpira kutembea chini. Tukalazimika kucheza mpira mrefu ambayo kwa bahati mbaya si aina yetu ya kucheza.”

“Tuliruhusu goli la kwanza kupitia makosa hayo hayo ya kiwanja. Tulijaribu kucheza mpira chini, tukafanya kosa rahisi la kuruhusu goli la kwanza lakini tukasawazisha. Tukaenda mapumziko tukiwa mabao 1-1. Kipindi cha pili tuliendelea kucheza vizuri tukiwa na mzani, tukiamini kwamba tunaweza kutengeneza nafasi nzuri ya kufunga bao la pili na kumaliza mechi. Kwa bahati mbaye tena ilitokea kona na tulifanya kosa kama timu tukaruhusu goli la pili.”

About Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

P